Utata
kuhusiana na uhalali wa tiba zinazotolewa na Dk. Juma Mwaka wa kituo
cha tiba mbadala cha Foreplan Clinic kilichopo Ilala jijini Dar es
Salaam unaelekea kuwa ‘pasua kichwa’ kwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dk. Hamis Kigwangalla, baada ya
majibu ya uchunguzi wa vyeti vya mganga huyo kushindwa kutolewa kwa umma
kama ilivyoahidiwa.
Awali, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wiki
iliyopita, Waziri Kigwangalla aliahidi kutoa taarifa kwa umma kuhusiana
na Dk. Mwaka juzi (Jumatatu). Alieleza hayo baada ya kufanya ziara ya
ghafla kwenye kituo cha Dk. Mwaka Desemba 14, 2015 na kutomkuta yeye na
baadhi ya watoa huduma wake kabla ya kumtaka (Dk. Mwaka) awasilishe
vyeti vyake wizarani kwa ajili ya ukaguzi.
Hata hivyo, licha ya Dk. Mwaka kutekeleza agizo alilopewa Desemba 16 na
waziri kukiri kuwa kweli vyeti hivyo vimefikishwa kwao na kuhakikiwa,
bado suala lake linaelekea kusumbua kwani hadi kufikia jana, hakukuwa na
ufafanuzi zaidi kama ilivyoahidiwa wiki iliyopita huku Dk. Kigwangalla
akiutaka umma utulie na kusubiri taarifa ya ukaguzi kwani hivi sasa kuna
masuala mengine ya kushughulikia.
“Tutawapa taarifa mara tutakapomaliza kuipitia ripoti hiyo, subirini tu kwa kuwa kuna kazi nyingi za kufanya wizarani,” Dk. Kigwangalla wakati alipoulizwa na mwandishi wa Nipashe jana kuhusiana na matokeo ya ukaguzi wav yeti mwaka kama alivyoahidi wiki iliyopita.
Akieleza zaidi, Dk. Kigwangalla alisema bado anaipitia ripoti hiyo na
akishamaliza, atashauriana na viongozi wengine wa wizara yao akiwamo
Waziri mwenye dhamana, Ummy Mwalimu, na kisha ndipo ataitisha mkutano na
waandishi wa habari kwa ajili ya kutoa taarifa.
ILIVYOKUWA
Desemba
14 ya wiki iliyopita, Dk. Kigwangalla alifanya ziara ya kustukiza
kwenye kituo cha Dk. Mwaka ambaye amekuwa maarufu kutokana na matangazo
mbalimbali anayotoa kila mara kuhusiana na tiba anazotoa.
Hata hivyo, baada ya Dk. Kigwangalla kufika kwenye kituo hicho,
hakumkuta Dk. Mwaka na wenzake na ndipo (Dk. Kigwangalla) alipotoa amri
ya kufungwa kwa muda kituo hicho akimtuhumu Dk. Mwaka na wenzake
kumkimbia na kisha akaamuru apeleke vyeti vyake ili vichunguzwe na kuona
kama huduma wanazotoa zinakidhi vigezo na ni salama kwa wagonjwa.
Desemba 20, Kigwangalla aliiambia Nipashe kuwa ameshapokea ripoti yenye
maelezo ya vyeti vya Dk. Mwaka na kwamba, angetoa ufafanuzi kwa vyombo
vya habari Jumatatu au Jumanne (juzi au jana).
-Nipashe

0 comments:
Post a Comment